Na enyi Waislamu! Jueni kuwa katika mali ya makafiri mliyo yateka, hukumu yake ni kugawiwa mafungu matano. Fungu moja ni la Mwenyezi Mungu na Mtume, na jamaa zake Mtume, na mayatima, nao ni watoto wadogo wa Waislamu waliofiwa na baba zao nao ni mafakiri; na masikini, nao ni wale Waislamu wenye haja; na msafiri, naye ni mwenye kukatikiwa safari yake ya halali. Na yaliyo khusishwa katika hiyo sehemu moja katika tano kuwa ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume hukhusishwa kwa maslaha ya umma kama anavyo pasisha Mtume katika uhai wake, au, baada ya kufa kwake, Imam. Na yaliyo baki katika ile Khumsi watapewa walio kwisha tajwa. Ama sehemu nne nyengine katika ghanima (ngawira), na Aya ikanyamaza kimya juu yake, ni za wale walio pigana. Basi jueni hayo, na myajue ikiwa mmemuamini Mwenyezi Mungu kweli, na mmeziamini Ishara tulizo mteremshia mja wetu, Muhammad, za kumthibitisha na kumsaidia, siku ya Mpambanuo, tulipo pambanua baina ya ukafiri na Imani, nayo ndiyo siku lilipo kutana kundi lenu na kundi la makafiri katika Badri. Na Mwenyezi Mungu Mwenye kudra kubwa juu ya kila kitu aliwapa ushindi Waumini juu ya uchache wao, kuwashinda makafiri juu ya wingi wao.