Enyi wenye kumsadiki Mwenyezi Mungu na Vitabu vyake na Mitume wake, wenye kuifuata Haki! Kunywa au kuvuta chochote kinacho lewesha, kucheza kamari, na kusimamisha mawe ya kutolea mihanga kwa ajili ya masanamu mnayo yaabudu, na kuagua kwa mishale, na mawe, na karatasi za kuagulia kudra iliyo ghaibu...yote hayo si chochote ila ni uchafu wa kiroho, na upotovu. Na hayo ni kupambiwa na Shetani tu. Basi yaachilieni mbali ili mpate kufuzu duniani kwa maisha bora, na Akhera mpate Janna yenye neema. Kuagua kwa mishale: ilikuwa ikiandikwa juu ya vijiti, kimoja kiliandikwa: "Mola wangu Mlezi kaniamuru", na kingine:"Mola wangu Mlezi kanikataza", na kingine hakikuandikwa kitu. Hutiwa vijiti hivyo katika mfuko kisha huchanganywa, na kohani hutia mkono wake akachomoa kimojapo, na akamjuvya mwenye kuuliza lilio aguliwa