Na Mwenyezi Mungu alimjaalia Nabii Isa na uwezo wa kusema na watu na ilhali yungali mtoto maneno ya kufahamika yenye hikima, kama alivyo sema nao utuuzimani mwake, bila ya tafauti katika hali hizo mbili. Na akawa katika miongoni walio jaaliwa kuwa ni watu wema.
Maryamu alisema kwa kustaajabu kupata mwana kwa njia isiyo ya kawaida: Vipi nitapata mwana na ilhali hapana mwanamume aliyenigusa? (yaani aliye lala nami). Mwenyezi Mungu Mtukufu akakumbusha kuwa Yeye huumba atakacho kwa kudra yake bila ya shuruti za sababu zilizo zowewa. Kwani Yeye akitaka jambo hulileta tu kwa taathira ya uwezo wake katika atakalo bila ya kutafuta kinginecho cha kutimiza matakwa yake.
Na atamtuma awe Mtume wake kwa Wana wa Israili, (Katika Injili ya Mathayo 15.24 Yesu anasema: Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.- Tazama pia Mathayo 10.5-6 na Mathayo 19.28 na Yohana 17.9) mwenye kutumia hoja za ukweli wa Utume wake kwa miujiza kutokana na Mwenyezi Mungu. Miujiza yenyewe ni kama kufanya kwa udongo sura ya ndege, kisha akipulizia vitaingia uhai na kutaharaki mithili ya ndege kwa atakavyo Mwenyezi Mungu. Pia ataponyesha, kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, walio zaliwa vipofu na wataona, na wenye maradhi ya ukoma waondokewe na ukoma, na walio onekana wamekwisha kufa wafufuke. Na yote hayo ni kwa idhini na matakwa ya Mwenyezi Mungu. Pia atawatajia wanacho weka akiba majumbani mwao, vyakula na vyenginevyo. Naye Nabii Isa awaambie: Ishara zote hizi Mwenyezi Mungu amezionyesha kwangu ili iwe hoja kuwa Utume wangu ni wa haki, ikiwa nyinyi ni katika watu wanao t'ii na kusadiki.(Katika Injili ya Yohana 5.30 Yesu anasema: Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe.)
Na mimi nimetumwa kwenu nisadikishe sharia ya Taurati aliyo teremshiwa Musa, na nikuhalalishieni, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, baadhi ya mliyo harimishiwa zamani. Na mimi nimekuja na ishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuthibitisha ukweli wa ujumbe wangu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nit'iini mimi.(Katika Injili ya Mathayo 5.17 Yesu anasema: Msidhani ya kuwa nilikuja kuitangua torati au manabii, la, sikuja kutangua, bali kutimiza.)
Kwani hakika Mwenyezi Mungu ametumiminia mimi na nyinyi kila namna ya wema, amenilea mimi na nyinyi, ni Mola Mlezi wenu na wangu mimi. Basi muabuduni Yeye tu. Na hii ndio njia isiyo kwenda ovyo.
Basi alipo kuja Isa a.s. akawaita watu wake wafuate Njia Iliyo Nyooka, wengi wao walikataa. Alipo yajua hayo aliwaelekea na kuwaambia: Ni nani atakaye nisaidia katika kazi hii niifanyayo ya kuitia kwenye Haki? Wakamjibu baadhi ya Waumini wenye kumuamini Mwenyezi Mungu na yeye: Sisi tunakuunga mkono, na tutakusaidia, kwa sababu wewe ni Mwitaji, unaita watu wende kwa Mwenyezi Mungu. Na shuhudia kuwa sisi tumemsafia Mwenyezi Mungu na ni wenye kufuata amri zake.