Na Musa alipo kwisha kuwa mtu mzima, na akakamilika, Mwenyezi Mungu alimpa hikima na ilimu. Na hisani kama hii tuliyo mpa Musa na mama yake, tunawapa wema wote kwa ajili ya wema wao.
Musa akaingia mjini Misri wakati walipo kuwa watu wake wameghafilika. Akawakuta watu wawili wanapigana. Mmoja ni katika Wana wa Israili, na mwengine katika kaumu ya Firauni. Yule Muisraili akamtaka msaada kumpiga khasimu yake. Naye Musa akamsaidia. Akampiga konde yule khasimu, akamuuwa bila ya kukusudia. Musa akajuta na akasema: Hakika mimi kuja kufanya kitendo hichi ni kazi ya Shetani. Hakika Shetani ni adui aliye wazi kwa uadui na kupoteza.
Musa akasema kwa kunyenyekea kwa Mwenyezi Mungu na majuto: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi nimejidhulumu nafsi yangu kwa niliyo yatenda. Basi nighufirie kitendo changu hichi. Mwenyezi Mungu akamuitikia ombi lake na akamsamehe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkuu wa kusamehe, Mkunjufu wa rehema.
Musa akasema kwa kunyenyekea: Ewe Mola wangu Mlezi! Kwa haki ya kunineemesha kwako kwa kunipa hikima, na ilimu, niwezeshe nitende kheri na yanayo faa. Ukiniwezesha hivyo basi kabisa sitakuwa msaidizi wa makafiri.
Kulipo pambazuka asubuhi Musa alikuwapo mjini, Misri, naye yumo katika khofu, akitaraji kufikiwa na madhara kutokana na watu kwa sababu vile alivyo muuwa Mmisri. Akamwona yule Muisraili aliye mtaka msaada jana, naye akamtaka msaada mara ya pili katika ugomvi na Mmisri mwengine. Musa akamkemea kwa kumwambia: Hakika wewe mtu matata mno, na dhaahiri wewe ni mpotovu. Unafanya yale yale uliyo yafanya jana, na unaniita tena nikusaidie!
Na Musa alipo taka kumtumilia nguvu Mmisri, ambaye ni adui wao wote wawili; kwa sababu ya uadui huu, yule mtu alidhani kuwa Musa atamuuwa, basi akasema: Unataka kuniuwa kama ulivyo muuwa mtu jana? Wewe hutaki ila kuwa muasi tu katika nchi, wala hutaki kuwa miongoni wanao lingania maslaha na kheri.
Akaja mtu mmoja Muumini katika kaumu ya Firauni kutoka mwisho wa mji, ilipo enea khabari ya Musa kumuuwa Mmisri. Yule mtu akamwambia Musa kwamba watu wanapanga kutaka kumuuwa. Akamwambia: Toka mji, ukimbie usije ukauliwa! Hakika mimi ni katika wanao kupa nasaha.
Musa akautoka mji naye amejaa khofu wasije maadui wakamdhuru, akimnyenyekea Mwenyezi Mungu amwokoe na udhalimu wa makafiri.